Jumatatu 22 Septemba 2025 - 23:57
Ukiachilia mbali adhabu, kwa nini hatutakiwi kufanya dhambi?

Hawza / Mtu anapofanya dhambi, hana budi kutumia neema zilezile ambazo Mwenyezi Mungu amempa ili amuabudu yeye; na hiki ni kitendo cha wazi cha kutokuwa na shukrani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Amirul-Mu’minin Imam Ali (a.s) katika Hekima ya 290 anasema jambo la kuzingatiwa sana kuhusu dhambi na adhabu:


«لَوْ لَمْ یَتَوَعَّدِ اللَّهُ عَلَی مَعْصِیَتِهِ، لَکَانَ یَجِبُ أَلَّا یُعْصَی شُکْراً لِنِعَمِهِ.»

Kama Mwenyezi Mungu asingewaonya waja wake kuhusu madhara ya maasi na dhambi, bado ingekuwa ni wajibu kutozifanya, ili kwa njia hiyo ionekane shukrani kutokana na neema Zake.

Sherehe:
Mwenye kufanya dhambi, kimsingi anaharibu neema za Mwenyezi Mungu alizopewa kwa ajili ya utiifu, ili mtu atende dhambi, anatumia nguvu na viungo vyote alivyoneemeshwa navyo na Mungu, ili hali Mwenyezi Mungu hakumpatia yeye nguvu hizo kwa ajili ya kumuasi na kutenda dhambi.
Mfikirie mtu anaekusudia kwenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu, anataka kufanya dhambi, kwa mfano, kuiba, Ili aitende dhambi hiyo, viungo vyote vya mwili wake vinapaswa kutekeleza majukumu yake kwa nguvu zote, ili aweze kuwa na uwezo wa kutenda kosa hilo.”

- Mapafu yake lazima yachukue hewa safi ili aweze kupumua na kuishi.

- Moyo wake lazima uendelee kudunda ili kusambaza damu mwilini kumuwezesha kuwa hai.

- Macho yake lazima yaone njia anayotaka kupitia.

- Miguu yake lazima itembee ili afike alikokusudia.

- Masikio yake lazima yasikie ili ajue hatari inayomkaribia.

- Mikono yake lazima ifanye kazi kufungua milango au kuchukua vitu.

- Ubongo wake lazima utoe amri kwenye viungo vyote na vitekeleze majukumu yao.


Ikiwa kiungo kimoja tu kisingefanya kazi, asingaliweza kufanya dhambi, yaani, kwa kila kosa analotenda, anatenda kwa kutumia neema za Mwenyezi Mungu ambazo hakupewa kwa ajili ya kumuasi bali kwa ajili ya utiifu.

Kwa hivyo, je, huoni kwamba mtu mwenye kutenda dhambi, kwa kila dhambi aitendayi anaflzipoteza nguvu na neema za Mungu?

Mwenyezi Mungu amewaonya waja Wake dhidi ya dhambi na amewaeleza adhabu, lakini hata lau asingewatahadharisha, bado binadamu hawakuwa na haki ya kuharibu neema hizo, kwa kila pumzi, kwa kila mpigo wa moyo, kwa uwezo wa kuona, kusikia, kufikiria na kutenda—mwanadamu ana wajibu wa kuwa mwenye kushukuru, na shukrani ya kweli ni kuepukana na maasi na kumtii Mola wake.

Imeknukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho: "Nasaha Fupi Kutoka katika Nahjul-Balagha"

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha